Tuesday, March 24, 2009

unamfahamu kiongozi anayetufaa

Mdau aliyejitambulisha kwa herufi 'R' anataja sifa za kiongozi. KIONGOZI ANAYETUFAA HUYU HAPA Kiongozi wa kweli:- ni mtumishi apendaye kwa hiari kuwatumika watu, siyo mtawala apendaye kwa ushawishi kutumikiwa na watu; Kiongozi wa kweli, maisha yake ni mfano tosha kwa kufuatwa na watu kwa hiari pasipo kujipendekeza au majigambo; Kiongozi wa kweli, hajinufasishi binafsi kupitia watu, bali ana uchungu wa shida za wengie na shauku ya kunufaisha maisha ya wengine Kiongozi wa kweli, ni matunda ya mtu yatokanayo na dhamira safi, tabia njema na upeo wa hali ya juu; Kiongozi wa kweli, ni msikivu, mwepesi wa kukiri mapungufu yake na hujiwajibisha mwenyewe pindi ashindwapo jambo pasipo visingizio; Kiongozi wa kweli, huwa tayari wakati wote kujifunza kutoka kwa watu wengine au jamii; Kiongozi wa kweli, hatofautishi kati ya maneno na matendo yake, siyo mnafiki wala kigeugeu Kiongozi wa kweli, hachukizwi na ushindani au upinzani bali huona ni changamoto na fursa pekee ya kujisahihisha na kujifunza ili kuelekea mahusiano bora na yenye faida kwa jamii. Kiongozi wa kweli, hapapariki wala kutapatapa apatwapo na matatizo, bali huwa jasiri na mwenye matumaini; Kiongozi wa kweli, hamiliki, hatawali wala hawi na amri juu ya watu, bali hushirikiana na kushauriana na watu anaowaongoza katika kuamua hatima yao na yake; Kiongozi wa kweli, hufurahia na kupongeza mafanikio ya wengine pasipo kuona gere na, husononeshwa na kusikitishwa na maanguko ya wengine Kiongozi wa kweli, mara nyingi haigi watu wengine, bali hubuni na kuvumbua mambo mapya yaliyo bora zaidi; Kiongozi wa kweli, wakati wote hutafuta maarifa, busara na hekima mpya na kamwe hathubutu kuhitimisha kujifunza katika maisha yake yote; Kiongozi wa kweli, hajilinganishi na wengine au kubweteka na mafanikio yake, bali hukazana kupanga na kutekeleza malengo na majukumu mapya anayojipangia kuelekea ubora endelevu na usiokoma kuboreka; Kiongozi wa kweli, wakati wote hurekebika, hukomaa, hukua na kujiendeleza kadri anavyoendelea kuongoza pasipo chembe yoyote ya ukaidi. Kiongozi wa kweli, huwa na mtazamo wa kuwajali binadamu wote waishio ulimwenguni, na hawi na mtazamo finyu usioona mbali.

No comments:

Post a Comment