Kukosa kuungwa mkono na wazazi, walezi pamoja na
kuamini kuwa kunahitajika nguvu kubwa katika utendaji wa kazi imedaiwa kuwa
chanzo cha wasichana kukimbia masomo ya sayansi na uhandisi.
Hayo yalisemwa na baadhi ya washiriki wa mafunzo ya
mafundi wa majokofu na viyoyozi kuhusu teknolojia mbadala za upozaji rafiki kwa
tabaka la Ozoni yanayofanyika katika Hoteli ya Paradise Jijini Mbeya.
Mkufunzi kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia
(Must), Moses Malole alisema kuwa imani kuwa kazi za uhandisi zinahitaji
matumizi ya nguvu pamoja na kutoungwa mkono na wazazi imekuwa ni kichochea cha
idadi kubwa ya wasichana kuyaepuka masomo ya uhandisi na sayansi.
Akitoa mfano alisema kati ya wasichana wanne waliokuwa
wanasoma masomo ya kozi ya awali ya uhandisi (Bridging course) kabla ya
kuungana na waliosoma diploma, wanafunzi watatu walijitoa katika kozi hiyo na
kuhamia katika kozi nyingine kwa kuhofia ugumu wa masomo.
Hata hivyo alisema kazi nyingi za uhandisi ikiwemo
ufundi wa majokofu hazitumii nguvu na kwamba kinachohitajika hivi ni kuongezeka
kwa juhudi za kuwahamasisha wasichana waweze kushiriki katika masomo ya sayansi
na uhandisi kwa kuwa ni rahisi na pia yanamanufaa katika jamii.
Kwa upande wake, Mkurugenzi msaidizi idara ya mazingira
kutoka ofisi ya Makamu wa Rais, Magdalena Mtenga alisema kuwa serikali imeanza
kuchukua juhudi za makusudi katika kuwahamasisha wasichana ili waweze kushiriki
katika masomo ya sayansi badala ya kuwa fani ya wanaume pekee.
Alisema baadhi ya juhudi imekuwa ni pamoja na
kuwasomesha ambapo hata hivyo alisema juhudi za pamoja kati ya serikali na
wananchi zinahitajika ili kuweza idadi kubwa ya wasichana kujiunga na masomo ya
sayansi.
Aidha
alisemawazazi na walezi wanatakiwa waunge mkono kwa kuwahamasisha
wasichana na si kuwakatisha tamaa kwa kuwaambia ni masomo magumu na
hawayawezi.
Warsha ya mafunzo ya mafundi wa majokofu na viyoyozi
inahusisha washiriki kutoka Mikoa ya Mtwara, Lindi, Mbeya, Rukwa, Katavi,
Ruvuma na Iringa hata hivyo kati ya washiriki wote hakuna mshiriki wa kike hata
mmoja.
No comments:
Post a Comment