Wakulima wilayani Chunya wameingiza shilingi bilioni 90
katika msimu wa kilimo uliopita kutokana na mauzo ya mazao ya ufuta,karanga,
alizeti na tumbaku.
Mkuu wa wilaya ya Chunya, Deodatus Kinawilo aliyasema
hayo alipokuwa akizungumza wakati wa ufungaji wa mafunzo ya kuvijengea uwezo
vikundi vya wakulima wa zao la alizeti wilayani humo.
Alisema kuwa kutokana na mapato hayo inadhihirisha kuwa
shughuli za kilimo zinamanyfaa kiuchumi kutokana na wakulima kuweza kupata
shilingi bilioni tisini katika msimu mmoja wa kilimo ambapo alisema kuwa
wananchi wanatakiwa kuacha kulalamikia ugumu wa maisha na badala yake wafanye
kazi.
Akitoa mchanganuo wa mapato hayo, Kinawilo alisema
wakulima wa alizeti walipata shilingi bilioni nne, ufuta bilioni 27, karanga bilioni
12 na tumbaku bilioni 47, hata hivyo alisema licha ya mapato hayo eneo
linalolimwa ni dogo ikilinganishwa na eneo linalofaa kwa kilimo.
Alisema eneo linalofaa kwa kilimo wilayani Chunya ni
kilomita za mraba 19,800 sawa na asilimia 66 na kwamba kati ya eneo hilo, eneo
linalotumika kwa kilimo ni kilomita za mraba 2,276 sawa na asilimia saba ambapo
alisema mkulima akijitahidi sana analima ekari mbili tu.
Aidha alisema mkulima wilayani humo akifuata kanuni
bora za kilimo anaweza kuvuna gunia 25 za kilo 60 kila moja kwa ekari, lakini
hivi sasa wanavuna kati ya gunia 4-12 kwa ekari.
Awali, Mkurugenzi wa Taasisi ya watetezi wa mazingira
na kilimo endelevu (KAEA), Lucas Malangalila alisema katika utafiti wa awali
walibaini kuwa kilimo cha zao la alizeti kinakabiliwa na changamoto nyigi
ikiwamo ukosefu wa soko la uhakika na uzalishaji mdogo wa wakulima, mbegu
zilizo chini ya kiwango pamoja na kukosekana kwa dhamira ya dhati ya wananchi
kuondokana na umasikini kupitia zao hilo.
Alisema baada ya kutambua changamoto zinazowakabili
wakulima, walivitambua vikundi vya wakulima na kuwapa mafunzo ya mwenendo wa
uongozi, masuala ya jinsia na kilimo cha mikataba na kuwakutanisha na wanunuzi
na wasindikaji.
No comments:
Post a Comment