Na Merali Chawe , Mbeya
Baadhi ya wakazi Mkoani Mbeya wameuomba uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mbeya kuwajengea jengo la kupumzikia wakati wakisubiri kuwaona wagonjwa wao ili kuepuka adha za mvua na jua kali.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, walisema kuwa kwa muda mrefu wamekuwa wakilazimika kukaa kwenye jua na wakati mwingine kunyeshewa na mvua wakati wakisubiri muda wa kuruhusiwa kuinia kuona wagonjwa wao.
Joseph Mwaisango alisema kuwa imefika wakati Uongozi wa Hospitali hiyo uangalie uwezekano wa kujenga jengo la kupumzikia watu wanaokuja kuwaona wagonja waliolazwa Hospitalini hapo.
« Baadhi ya watu wanaokuja kuna wagonjwa wanatoka nje ya mji, hivyo wakija asubuhi wanalazimika kubakia hadi mchana , lakini kukosekana kwa jengo la kupumzikia wanalazimika kukaajuani na wakati mwingine kunyeshewa na mvua » alisema.
Eliza John alisema waathirika zaidi wa ukosefu wa jengo hilo kunawaathiri zaidi wanawake wanaokuwa wamekwenda na watoto ambapo alisema imefika wakati kwa Hospitali kuwafikiria watu wanaokuja kuwaona wagonjwa Hospitalini hapo.
Akizungumzia suala hilo, Katibu wa Hospitali ya Rufaa Mbeya Aisha Mtanda alisema kuwa uongozi wa Hosptali unatambua kuwepo kwa tatizo la ukosefu wa jengo la kupumzikia, lakini tatizo la ukosefu wa fedha ndio kikwazo cha kufanikisha ujenzi wa jengo hilo.
« Tunatambua uwepo wa tatizo na katika vikao huwa tunaijadili, lakini tatizo linalotukaili kwa muda mrefu ni ukosefu a fedha za kutekeleza ujenzi wa jengo hilo la kupumzikia watu wanaokuja kuona wagonjwa » alisema.
Wakati uo huo, Mtanda amewataka wananchi wanaokwenda kuona wagonjwa kutoingia na watoto Hospitalini hapo ili kuwaepusha na magonjwa ya kuambukiza.
« Sio vizuri kuingia na watoto katika maeneo ya huduma sababu ya maambukizi,watu wazima wanaelekezwa sehemu ya kunawa ili wasiwaambukize wengine huko wanakokwenda lakini kwa watoto vigumu » alisema
No comments:
Post a Comment