Wednesday, February 12, 2014

Wasomi watakiwa kutotumia jazba kujadili masuala ya muungano

Na Merali Chawe, Mbeya

Wasomi nchini wametakiwa kujadili hoja za muungano kwa umakini na busara na waepuke jazba ambazo hazina maslahi kwa Taifa.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro aliyasema hayo alipokuwa akifungua Kongamano la wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu vilivyopo Mkoani hapa lillojadili tathmini ya miaka 50 ya utekelezaji wa masuala ya Muungano.

Alisema wasomi wanatakiwa kujadili hoja za Muungano kwa kuwa makini, wastahmilivu na wawe makini kutoa maoni kwa manufaa makubwa na mustakabali wa Taifa.


« Hapa mmekutana wasomi kutoka vyuo mbalimbali, hivyo muwe watulivu mnapotoa maoni yeu katika kujadili tathmini ya miaka 50 ya utekelezaji wa masuala ya muungao, vininevyo mkijadili kwa jazba unaweza kuongea utumbo na wenzako wakashangaa » alisema .

Katika hatua nyingine, Kandoro aliwataka Watanzania kuilinda amani iliyopo nchini kwa kuwa ndiyo inayowezesha watu kufanya shughuli zao za biashara, kilimo, uchumi na kisiasa bila ya usumbufu wowote.

« Inashangaza kuona baadhi ya watu wanasema amani ikivunjika liwalo na lwe, ndugu zangu Tanzania ni nchi yetu na kama kukitokea uvunjifu wa amani kule tutaokimbilia hatutakuwa Watanzania tena bali tutaitwa wakimbizi » alisema na kuongeza kuwa kama kunatofauti zinazojitokeza ni bora kujadiliana.

Kongamano hilo la siku moja liliandaliwa na ofisi ya Makamu wa Rais na kuwashirikisha wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu vilivyopo Mkoani hapa ambapo baadhi ya mada zilizowasilishwa ni kuhusu Muungano ni masuala ya Kisiasa, Kiuchumi na Kisheria.

No comments:

Post a Comment